RAIS WA CHAMA CHA WAUGUZI TANZANIA (TANNA) ATETA NA WAUGUZI WA HOSPITALI YA MWANANYAMALA
Posted on: June 25th, 2025
Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA), Dkt. Ezekiel Mbao, leo Juni 26, 2025 ametembelea wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala na kufanya kikao maalum kwa lengo la kusikiliza changamoto za wauguzi hao pamoja na kuhimiza mshikamano na uanachama ndani ya chama hicho.
Akizungumza na wauguzi hao, Dkt. Mbao amesisitiza umuhimu wa wauguzi wote kuwa wanachama hai wa TANNA, akibainisha kuwa chama hicho ndicho chombo rasmi cha kusimamia na kutetea maslahi ya wauguzi nchini hivyo kuwasihi wale ambao bado hawajajiunga na chama hicho, kuchukua hatua na kujiunga kwa ajili ya manufaa yao ya sasa na baadaye.
“Tunahitaji kuwa wamoja na kuwa na sauti moja, TANNA ni jukwaa letu la pamoja la kuhakikisha kwamba changamoto zinazotukabili katika utendaji kazi zinapata majibu ya msingi, mnapokuwa wanachama hai mnakuwa na nguvu ya pamoja ya kutetea haki zenu,” amesema Dkt. Mbao.
Aidha amesema kuwa chama hicho kinaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kusaidia wauguzi katika kutatua changamoto za kibinafsi zinazojitokeza wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku, ikiwa ni hatua inayolenga kuongeza ari na motisha kwa wauguzi katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.