"KILA MTUMISHI ATIMIZE WAJIBU WAKE KWA NAFASI YAKE ILI KUONGEZA UFANISI KATIKA KUTOA HUDUMA"- DR. BENELA.

Posted on: June 18th, 2025

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dkt. Zavery Benela, ametoa wito kwa watumishi wa hospitali hiyo kutimiza majukumu yao kwa weledi na uadilifu kila mmoja kwa nafasi yake ili kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.


Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa kufunga mwaka wa watumishi wa hospitali hiyo uliofanyika Juni 18, 2025, Dkt. Benela amesema kuwa mafanikio ya Hospitali hiyo yanaenda sambamba na kiwango cha mshikamano na uwajibikaji wa mfanyakazi mmoja mmoja katika nafasi yake.



“Ni muhimu kila mmoja wetu kujitathmini na kuona namna anavyotekeleza wajibu wake kwa kuzingatia maadili ya kazi na dhamira ya kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema Dkt. Benela.


Katika kikao hicho, watumishi wamepata fursa ya kujadili mafanikio yaliyofikiwa katika mwaka mzima huku wakipendekeza mikakati mbalimbali ya kuboresha mazingira ya kazi na huduma bora kwa wagonjwa.



Akizungumzia kuhusu mipango ya Hospitali hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Dkt. Benela ameeleza kuwa vipaumbele vimewekwa katika maeneo muhimu ikiwemo kuboresha miundombinu ya utoaji huduma, huku akiwataka viongozi wa vitengo na idara zote kuhakikisha wanafuatilia utekelezaji wa mipango hiyo kwa karibu na kutoa mrejesho wa mara kwa mara, ili kuhakikisha mwelekeo wa Hospitali unaendana na matarajio ya Serikali na wananchi kwa ujumla.


Kwa upande wake Afisa Utumishi wa Hospitali ya Mwananyamala, Bw. Obeid Ilomo amewataka watumishi wote kuendelea kufanya kazi kwa nidhamu, bidii na uadilifu kama nyenzo muhimu katika kufanikisha malengo ya hospitali hiyo.



“Tuendelee kushirikiana kwa karibu, kila mmoja achukue jukumu la kuhakikisha anatimiza wajibu wake kikamilifu kwa manufaa ya jamii inayotegemea huduma zetu” ameeleza Bw. Ilomo